Mrepublican Donald Trump atakuwa rais ajaye wa Marekani – baada ya kupata ushindi wa kihistoria ambao umemrejesha tena katika Ikulu ya White House.
Kinyang’anyiro kati yake na mgombea wa chama cha Democratic Kamala Harris kilidhaniwa kuwa cha ushindani mkali lakini matokeo ya uchaguzi yalionyesha kuwa Trump amepata kura za kutosha kupata ushindi.
Atakuwa rais wa kwanza wa zamani kurejea madarakani kwa zidi ya miaka 130, akiwa na miaka 78 – kuchaguliwa katika wadhifa huo.
Matokeo ya uchaguzi yatathibitishwa lini?
Viongozi wa dunia tayari wampongeza Trump kwa ushindi wa uchaguzi wa rais Marekani miongoni mwao Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mwenzae wa Uingereza Keir Starmer, lakini matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais hayajathibitishwa.
Kulikuwa na hofu kwamba ushindani mkali kati ya wagombea katika baadhi ya majimbo muhimu ungeibua maswali mengi kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.
Lakini mambo yaligeuka ghafla katika majimbo ya North Carolina, Georgia, Pennsylvania na Wisconsin, pamoja na ushindi katika majimbo ambayo yamekuwa yakiunga chama cha Republican, ulimuwezesha Trump kufikia idadi ya kura 270 ya wawakilishi maalum wanaohitajika kushinda uchaguzi wa urais.
Kituo cha CBS, mshirika wa utangazaji wa BBC nchini Marekani kilikadiria Donald Trump kuwa mshindi wa uchaguzi huo mwendo wa 05:30 EST (10:30 GMT) sikumoja baada ya uchaguzi.
Hata hivyo matokeo ya kina huenda yakachukuwa siku au hata wiki kadhaa kuthibitishwa katika kila jimbo.
Je, Donald Trump sasa ni Rais?
Hapana. Trump sasa ni rais mteule, na mgombea mwenza wake JD Vance anakuwa makamu wa rais mteule.
Trump ataapishwa Jumatatu, tarehe 20 Januari 2025, ambapo atachukuwa rasmi hatamu ya uongozi na majukumu ya urais kisheria..
Nini kitafanyika kati ya siku ya uchaguzi na siku ya kuapishwa?
Mara baada ya kura zote sahihi kuhesabiwa na matokeo ya mwisho kutangazwa, wawakilishi maalum wanaofahamika kama Electoral College watathibitisha matokeo yauchaguzi.
Katika kila jimbo idadi tofauti ya kura za wawakilishi maalum zinagombaniwa. Kuzungumkuti ni kupata kura hizo – na sio tu kuungwa mkono na wapiga kura wenyewe – kwani wawakilishi hao maalum ndio hatimaye huamua mshindi.
Kwa ujumla, majimbo hutoa kura zote za wawakilishi maalum kwa yeyote atakayeshinda idadi kubwa ya wapiga kura, na hii inathibitishwa baada ya mikutano ya tarehe 17 Desemba.
Bunge jipya la Marekani litakutana tarehe 6 Januari kuhesabu kura za wawakilishi maalum na kumthibitisha ramsi rais mpya.
Ni kikao hicho cha bunge cha kuthibitisha matokeo ya uchaguzi, ambapo wafuasi wa Trump walijaribu kuvuruga, walipoandamana hadi majengo ya Bunge la Marekani mwaka 2021 baada ya Trump kukataa kukubali kushindwa kwa Joe Biden.
Rais mteule na Makamu wa Rais mteule sasa watafanya nini?
Rais mteule Trump na makamu wa rais mteule JD Vance watafanya kazi na timu yao ya mpito kuandaa makabidhiano hayo kutoka kwa utawala wa Rais Biden.
Watabainisha vipaumbele vyao vya sera, kuanza kuhakiki wagombeaji ambao watachukua majukumu muhimu katika utawala mpya, na kujiandaa kuchukua majukumu ya serikali.
Trump na timu yake pia wataanza kupokea taarifa za siri za usalama wa taifa zinazohusu vitisho vya sasa na operesheni zinazoendelea za kijeshi.
Rais mteule na makamu wa rais mteule pia wanapata ulinzi wa lazima kutoka kwa Idara ya Huduma ya usalama (Secret Service) ya Marekani.
Rais anayeondoka kwa kawaida humwalika rais mteule katika Ikulu siku chache baada ya uchaguzi.
Pia kwa kawaida huhudhuria hafla ya uapisho wake kuashiria makabithiano ya madaraka kwa amani, ingawa Trump aliamua kususia hafla hiyo mnamo 2020.
Hata hivyo alifuata desturi iliyoanzishwa na Ronald Reagan ya kuacha barua iliyoandikwa kwa mkono katika Ofisi ya Oval ili mrithi wake aisome.
Wakati huo, Rais Biden aliwaambia waandishi wa habari kwamba mtangulizi wake alikuwa ameacha “barua ya ukarimu sana”.
Baada ya kuapishwa, rais mpya anaanza kazi mara moja.