Trump ashinikiza Ukraine kukubaliana na Urusi kusitisha vita

Trump anatarajiwa kukutana na Rais Zelenskyy wa Ukraine leo Jumatatu baada ya kukutana na Rais Putin wa Urusi juzi Jumamosi.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais Donald Trump wa Marekani (kulia) na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House.

Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza shinikizo kwa Ukraine kukubali makubaliano ya kumaliza vita na Urusi, akidai kwamba Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anaweza kuchagua kumaliza mzozo huo yamkini mara moja.

Akimzungumzia Zelenskyy siku moja kabla ya ziara yake muhimu katika Ikulu ya Marekani siku ya Jumatatu, Trump alionya kwamba kurejeshwa kwa eneo la Crimea lililokaliwa na Urusi na uanachama wa Ukraine katika Umoja wa Kujihami wa Nchi za Kaskazini mwa Atlantiki, NATO hakutakuwa sehemu ya makubaliano yoyote ya maelewano.

“Rais Zelenskyy wa Ukraine anaweza kumaliza vita na Urusi yamkini mara moja, ikiwa anataka, au anaweza kuendelea kupigana,” Trump alisema kwenye mtandao  wake wa Truth Social siku ya Jumapili.

Matamshi ya Trump yanajiri wakati viongozi wa Ulaya wanatarajiwa kuandamana na Zelenskyy katika ziara yake mjini Washington, DC leo Jumatatu huku kukiwa na wasiwasi mjini Brussels na Kyiv kwamba Rais wa Marekani anaweza kukubali makubaliano yanayomfaidi sana Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Akizungumza muda mfupi baada ya matamshi ya Trump siku ya Jumapili, Zelenskyy alisema kuwa ustahimilivu wa awali kwa Moscow, ikiwemo kuhusu Crimea, ulimtia moyo Putin kuanzisha vita zaidi.

“Sote tuna hamu kubwa ya kumaliza vita hivi haraka na kwa njia ya kuaminika. Na amani lazima iwe ya kudumu,” Zelenskyy alisema katika chapisho kwenye X.

“Si kama ilivyokuwa miaka iliyopita, wakati Ukraine ililazimishwa kuachia Crimea na sehemu ya Mashariki mwetu – sehemu ya Donbas – na Putin akaitumia kama ngazi ya shambulio jipya. Au wakati Ukraine ilipewa kile kilichoitwa ‘dhamana za usalama’ mwaka 1994, lakini hazikufanya kazi.”

Zelenskyy aliongeza kuwa Crimea “haikupaswa kuachwa wakati huo, kama vile Waukraine hawakutoa Kyiv, Odesa, au Kharkiv baada ya mwaka 2022”.

“Waukraine wanapigania ardhi yao, kwa ajili ya uhuru wao,” alisema.

Wakati Trump ameashiria kuwa makubaliano na Moscow yatajumuisha kubadilishana maeneo fulani ya ardhi kati ya Urusi na Ukraine, Zelenskyy amekataa vikali mara kwa mara kukabidhi eneo lolote la Ukraine kwa “mvamizi”.

Website |  + posts
Share This Article