Timu ya taifa ya soka ya wavulana wasiozidi umri wa miaka 15 yatajwa

Kocha mkuu Patrick Nyale amekitaja kikosi hicho cha wachezaji 14, kitakachoshiriki mashindano hayo yatakayoanza tarehe 22 hadi 30 mwezi Oktoba.

Tom Mathinji
1 Min Read

Timu ya taifa ya soka ya wavulana wasiozidi umri wa miaka 15 itakayoshiriki kwenye makala ya kwanza ya mashindano ya dunia Jijini Baku, Azerbaijan, imetajwa.

Kocha mkuu Patrick Nyale amekitaja kikosi hicho cha wachezaji 14, kitakachoshiriki mashindano hayo yatakayoanza tarehe 22 mwezi Oktoba hadi tarehe 30 mwezi Oktoba.

Nahodha wa timu hiyo atakuwa kiungo Innocent Media, huku wachezaji wengine wakiwa mlindalango Elvis Odhiambo, walinzi Alpha Omega na Junior Otieno, wachezaji wa kati Silas Juma na Javan Ochieng na washambulizi Duncan Muya na Roy Clinton.

Jopo la shirkisho la FIFA lilikubaliana kuanzisha mashindano hayo kuwapa fursa zaidi chipukizi wasiozidi umri wa miaka 15, lakini watatumia uwanja mdogo, mechi zitakuwa za dakika 20 kila kipindi na zitachezwa na wachezaji wanane-wanane.

Mashindano ya kwanza ya wavulana yataandaliwa mwaka huu, ya wasichana mwaka ujao na wote kuanzia mwaka 2028. Timu hiyo ya Kenya itaondoka humu nchini kuelekea nchini Azerbaijan kesho.

Share This Article