Sheebah Karungi akabiliwa na madai ya kuiba wimbo

Mwanamuziki chipukizi Dwiz Playboy anadai kwamba Karungi alinakili wimbo wake uitwao Bukutu.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki nyota wa kike nchini Uganda Sheebah Karungi, amejipata pabaya baada ya kuandamwa na madai ya wizi wa wimbo, kutoka kwa mwanamuziki chipukizi Dwiz Playboy.

Playboy anadai kwamba Karungi alinakili wimbo wake uitwao Bukutu, kufuatia kutolewa kwa wimbo mpya wa Sheebah akishirikiana na mwimbaji mwenzake Karole Kasita.

Tuhuma hizo zimeibuka siku chache baada ya wasanii hao wawili mashuhuri kuungana na kutoa wimbo wao wenye jina hilo hilo, Bukutu, ambao umekuwa ukivutia hisia za mashabiki katika tasnia ya burudani nchini Uganda.

Dwiz Playboy, anasema alitoa wimbo wake mwaka 2025 na kuupakia kwenye majukwaa ya muziki mtandaoni, ikiwemo YouTube.

Alisema alishangazwa kuona Sheebah akitoa wimbo wenye jina linalofanana na la wimbo wake.

Katika mahojiano, mwimbaji huyo chipukizi pia alieleza safari yake ya muziki, akifichua kuwa yeye na meneja wake walikuwa wachezaji wa soka kabla ya kuamua kuachana na soka na kuingia rasmi katika muziki.

Dwiz anadai kuwa walipoamua kuanza muziki, walimfuata Sheebah wakati wa uzinduzi wa Karma Music kwa ajili ya kufanya majaribio ya kuonyesha vipaji vyao. Anaamini kuwa alikuwa miongoni mwa waliofanya vizuri zaidi.

Anahisi kuwa kutolewa kwa wimbo wa Sheebah na Karole Kasita kumedhoofisha maendeleo ya kazi yake, huku umaarufu wa wimbo wao ukifunika kazi yake mwenyewe.

Sheebah Karungi na Karole Kasita bado hawajajibu hadharani tuhuma hizo.

Share This Article