Mkurugenzi mtendaji wa tume ya filamu nchini Kenya, KFC, Timothy Owase amehimiza wabunifu kuhusika katika mchakato wa kushirikisha umma kuhusu sheria iliyopendekezwa ya uchumi wa ubunifu.
Akizungumza kwenye video iliyochapishwa na KFC kwenye mitandao ya kijamii, Owase alielezea kwamba Mswada huo umewasilishwa bungeni na serikali lakini unalenga kulainisha kazi za wabunifu katika nyanja mbali mbali.
Kutokana na hilo, Mkurugenzi huyo mtendaji wa KFC amehimiza wabunifu kuhakikisha kwamba wanatoa maoni yao katika vikao vya kushirikisha umma.
Kulingana na Owase, mapendekezo yaliyo kwenye mswada huo ulivyo wa sasa yalitokana na utafiti wa kina uliofanywa katika sekta ya ubunifu nchini,
Mswada unaopendekezwa wa Sheria ya Uchumi wa Ubunifu unapanua wigo wake zaidi ya utengenezaji wa filamu na kujumuisha sekta pana ya ubunifu, ikiwemo sanaa za maonyesho, mitindo ya mavazi, michezo ya kidijitali na taaluma nyingine za ubunifu.
Kwa taasisi kama Tume ya Filamu Kenya hili linaashiria umuhimu wa kuimarisha mifumo, ushirikiano na huduma za usaidizi zinazowawezesha wabunifu na biashara zao kukua na kufanikiwa.
Owase anasema sheria hiyo itasaidia katika kuweka uwazi katika shughuli za biashara na fursa za ufadhili na kuhakikisha ushiriki wa maana wa wananchi katika mchakato wa kutunga sheria inayokidhi mahitaji ya wabunifu.