Timu ya Nairobi United yapata ufadhili wa shilingi milioni 50

Tom Mathinji
2 Min Read
Wakfu wa Johnson Sakaja kufadhili timu ya Nairobi United.

Timu ya soka ya Nairobi United ina sababu ya kutabasamu baada ya kupata ufadhili wa shilingi milioni 50 kutoka kwa wakfu wa Johnson Sakaja.

Akizungumza wakati wa warsha ya kuikabidhi timu hiyo kwa wakfu wa Sakaja katika ukumbi wa City Jijini Nairobi, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alisema kupitia wakfu huo, mahitaji yote ya wachezaji yatashughulikiwa, ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, ukuzaji talanta na elimu.

“Mimi ni mshindani mkuu na ninapenda kushinda. Natarajia nidhamu, kujitolea na umoja kutoka kwa timu nzima,” alisema Sakaja.

Alisema anawatafuta wachezaji bora, huku akiwahimiza kufanya mazoezi kwa bidii, ili waweze kudumisha nafasi yao sasa.

Wakfu wa Johnson Sakaja kufadhili timu ya Nairobi United.

“Kwa sasa tunawekeza katika michezo. Tuna vituo vya michezo Dandora na Woodley,” alisema Gavana huyo.

Gavana huyo alisema shindano la Sakaja Super Cup litang’oa nanga Oktoba 1, 2024, akidokeza kuwa awamu hii ya pili itakuwa bora zaidi.

“Awamu hii ya pili itakuwa kubwa na bora. awamu iliyopita ilikuwa na timu 340, lakini wakati huu tutakuwa na timu 780 Jijini Nairobi,” alidokeza Gavana huyo.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa timu ya Nairobi United Samuel Born Maina, alihakikisha kujitolea kwake kuunga mkono timu hiyo akisema atashikilia maono ya timu hiyo.

Share This Article