Thang’wa apinga kuongezwa kwa muhula wa viongozi

Marion Bosire
1 Min Read
Karungo wa Thang'wa, Seneta wa Kiambu

Seneta wa kaunti ya Kiambu Karungo wa Thang’wa amewasilisha katika bunge la Seneti stakabadhi ya kumbukumbu inayopinga mpango wa kuongeza muhula wa viongozi waliochaguliwa.

Thang’wa badala yake anapendekeza marekebisho katika sheria ili kupunguza muda wa muhula wa viongozi waliochaguliwa hadi miaka minne.

Mswada wa kuongeza muhula wa viongozi kutoka miaka mitano hadi miaka saba uko katika bunge la taifa na kwa sasa uko katika kiwango cha kushirikisha umma.

Wakenya wana muda hadi Ijumaa kuwasilisha maoni yao kuhusu mswada huo wa Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei wa chama cha UDA.

Chama hicho hata hivyo kimejitenga na mapendekezo ya Cherargei kikiyataja kuwa yake binafsi na wala sio msimamo wa chama.

Mchakato wa kushirikisha umma katika mswada huo wa kurekebisha katiba wa mwaka 2024 umekuwa ukiendelea tangu Oktoba 2, 2024.

Iwapo mswada huo utapitishwa, muhula wa kuhudumu wa Rais na viongozi wengine utaongezwa kutoka miaka mitano ya sasa hadi miaka saba.

Thang’wa ambaye ni mmoja wa viongozi wanaopinga wazi kubanduliwa kwa naibu rais Rigathi Gachagua mamlakani, amewasilisha pia mswada wa kulainisha mchakato wa kubandua mamlakani viongozi.

Lengo lake anasema ni kuhakikisha kwamba mchakato huo unatekelezwa kwa njia wazi na ya haki.

 

Share This Article