Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi nchini Myanmar, imeongezeka hadi 1,000, huku watu zaidi ya 2,000 wakijeruhiwa.
Tetemeko hilo la ardhi ambalo pia liliathiri nchini jirani ya Thailand lilikuwa la kiwango cha 7.7.
Kulingana na vyanzo vya habari nchini Myanmar, wengi wa waliofariki walikuwa mjini Mandalay, ambao ndio mji wa pili kwa ukubwa na ndio uliokuwa karibu sana na kitovu cha tetemeko hilo.
Shughuli za uokoaji zinaendelea katika eneo la juu ambalo halijakamilika huko Bangkok baada ya kuporomoka, na takriban wafanyakazi 100 wa ujenzi hawajulikani waliko na sita wamekufa, kulingana na maafisa wa serikali ya eneo hilo.
Serikali ya kijeshi ya Myanmar imetoa ombi la msaada wa kimataifa, ombi adimu kutoka kwa serikali iliyojitenga na ambayo imewekewa vikwazo vikali na mataifa ya Magharibi katika miaka ya hivi karibuni.
Udhibiti mkali wa jeshi la Myanmar na kuendelea kukosekana kwa utulivu wa ndani kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kunafanya kuwa vigumu kupata taarifa sahihi kuhusu maafa hayo.