Wenyeji Ivory Coast walijizatiti kisabuni na kuwavua ubingwa Senegal baada ya kuwalemea kwa mabao 5-4 na kufuzu kwa robo fainali kupitia matuta ya penalti baada ya timu zote kuambulia sare ya 1-1 katika dakika 120.
Habib Diallo aliwaweka Simba wa Teranga kifua mbele kunako dakika ya 4 ya mechi hiyo ya awamu ya 16 bora, akiunganisha pasi ya Sadio Mane.
Tembo wa nyumbani walijituma na kuendelea kumiliki mpira kwa kipindi kirefu na mashambulizi tele yaliyozaa matunda baada ya kupata penalti ya 86 iliyofungwa na nahodha Frankie Kessie na kulazimisha muda wa mazidadi.
Katika hatua ya matuta, Ivory Coast waliunganisha mikwaju yote huku beki Moussa Niakhate akigonga chuma.
Ilikuwa mara ya saba mtawalia kwa mabingwa watetezi wa AFCON kushindwa kufuzu kwa hatua ya robo fainali.