Stima Sacco yazindua tawi jipya katikati ya jiji la Nairobi

Marion Bosire
2 Min Read

Chama cha Akiba na Mikopo cha Stima, Stima Sacco kimezindua tawi jipya katikati ya jiji la Nairobi katika jumba la Electricity House.

Hatua hii inanuiwa kupeleka huduma za chama hicho karibu na wateja.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa tawi hilo, Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho Dr. Gamaliel Hasan alisema uzinduzi huo ni ishara ya kujitolea kwa Stima Sacco kushughulikia mahitaji yanayobadilika kila kuchao ya wanachama wake pamoja na mahitaji ya kisasa ya kidigitali hasa jijini Nairobi.

“Nairobi ndio mji mkuu wa kibiashara wa Kenya ambao umejikita katika uvumbuzi, ujasiriamali na sekta kubwa ya kifedha. Kwa sababu hiyo, sio jambo la kushtua kwamba Nairobi ina sehemu nyingi za kifedha za kuchagua ili kukidhi mahitaji na malengo ya wakazi wake.” alisema Dr. Hassan.

Alisisitiza kwamba mpango wa upanuzi wa chama hicho umejikita kwenye nguzo tatu muhimu ambazo ni upatikanaji, urahisishaji na kutosheleza wanachama.

Mhandisi Albert Mugo ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa Stima Sacco alisema kwamba kuzinduliwa kwa tawi jipya kunaonyesha kuendelea kujitolea kwa chama hicho kama mshirika mkuu katika maendeleo ya kiuchumi na kifedha ya nchi.

Kulingana naye, ufunguzi wa tawi jipya ni hatua muhimu katika kutekeleza mpango mahsusi wa chama wa mwaka 2019-2024 unaohusisha upanuzi.

Kando na afisi kuu jijini Nairobi, Stima Sacco ina matawi katika miji kama vile Nakuru, Mombasa, Kisumu, Eldoret, Nairobi, Olkaria, Embu, Meru, Kisii na hili la hivi punde zaidi katika jumba la Electricity jijini Nairobi.

Website |  + posts
Share This Article