Mwanamuziki wa kike wa mtindo wa reggae kutoka Jamaica Shauna McKenzie maarufu kama Etana ametangaza kuahirishwa kwa tamasha lake lililokuwa liandaliwe Jumamosi Disemba 7, 2024.
Akizungumza kwenye video iliyosambazwa mitandaoni, Etana ambaye yuko nchini Kenya alilalamikia kile alichokitaja kuwa hujuma akisema onyesho lake lilitangazwa kwa muda mrefu kabla ya lile la Diamond Platnumz.
Kulingana naye, waandalizi walilazimika kufutilia mbali tamasha lake kwani matamasha mawili makubwa hayawezi kuandaliwa katika eneo moja kwa kile walichokitaja kuwa sababu za kiusalama.
Etana anasema alihisi kudharauliwa kama mwanamke na mwanaume kupatiwa kipaumbele lakini amesisitiza kwamba hafi moyo.
Tarehe mpya ya tamasha lake aliahidi itatangazwa leo huku akiomba radhi mashabiki zake ambao walikuwa wamejiandaa kupokea burudani kutoka kwake.
Alisimulia jinsi Diamond alifika kwenye kipindi fulani cha runinga ambapo walihojiwa akiwa na halaiki ya watu akisema hakushtuliwa na hilo kwani nchini Jamaica, ni kawaida kwa wasanii kuja na watu wengi.
Etana alishangaa ni kwa nini wanaume wengi waliungana dhidi yake mwanamke mmoja huku Kenya ikiendelea kuadhimisha siku 16 za uanaharakati dhidi ya dhuluma za kijinsia.
Mwimbaji huyo hata hivyo anatizamia kutumbuiza mashabiki zake jijini Nairobi hivi karibuni huku akiwahakikishia kwamba ataendelea kuwapenda daima.
Matamasha yake mengine kwenye ziara yake nchini iitwayo “Pamoja Tour” hata hivyo yataendelea ambapo Disemba 11, 2024, atakuwa huko Mombasa, Disemba 13 atumbuize huko Meru na Disemba 15 atakuwa jijini Eldoret.