Wizara ya kilimo imehakikisha kuwa taifa hili lina mahindi ya kutosha, baada ya kushuhudia mavuno yaliyoimarika mwaka 2023.
Waziri wa kilimo Andrew Karanja, amedokeza kuwa zaidi ya magunia miliono 60 ya mahindi yalivunwa mwaka jana hapa nchini, kutokana na hali nzuri ya hewa na upatikananji wa mbolea ya gharama nafuu.
Kulingana na waziri Karanja, kutokana na mvua kubwa iliyoshuhudiwa hapa nchini mapema mwaka huu, mavuno ya mahindi yanatarajiwa kufika magunia miliono 70.
“Zaidi ya magunia Milioni 60 ya mahindi yalivunwa mwaka 2023, lakini kutokana na hali nzuri ya hewa mwaka huu, tunatarajia kuvuna zaidi ya magunia milioni 70 ya mahindi,” alisema waziri huyo.
Karanja alisema kuwa serikali imenunua magunia milioni 1.5 ya mbolea ya gharama nafuu, kupiga jeki shughuli za kilimo wakati wa msimu ujao wa mvua za vuli.
Aliwahimiza wakulima kuchukua fursa ya msimu wa mvua za vuli kupanda mimea kutumia mbolea za gharama nafuu.
“Tunazo mbolea ya gharama nafuu, itakayouzwa kwa wakulima wanapojiandaa kwa msimu ujao wa mvua. Gunia moja ya kilo 50 ya mbolea hiyo itauzwa shilingi 2,500, na zinapatikana katika vituo vyote vya halmashauri ya nafaka na mazao NCPB,” aliongeza waziri huyo.
Aliongeza kuwa wizara yake inashirikiana na serikali za kaunti kuhakikisha mbolea hiyo inawafikia wakulima kwa urahisi.