Muungano mkuu wa upinzani nchini Sudan Kusini umeonekana kugawanyika, hali inayozidisha mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.
Kiongozi wa chama cha upinzani SPLM-IO, Dkt. Riek Machar, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini kufuatia makubaliano ya amani yaliyolenga kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir, aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani mwezi uliopita.
Hapo jana, kundi la viongozi waandamizi wa SPLM-IO lilitangaza nia ya kumteua Stephen Par Kuol kuwa kiongozi wa mpito hadi pale Dkt. Machar atakapokuwa huru.
“Tulichofanya ni kutatua mgogoro huu wa uongozi ambao umesababishwa na mgogoro unaotokana na kuwekwa kizuizini kwa mwenyekiti wetu na kutoroka kwa viongozi wetu wengine kama naibu mwenyekiti na katibu mkuu,” alisema Par.
Hata hivyo, hatua hiyo ilipingwa na baadhi ya wajumbe wa chama hicho, huku Par Kuol akilazimika kujitetea dhidi ya madai kwamba alikuwa anatekeleza mapinduzi ya kisiasa ndani ya chama.
Ikiwa ni wiki mbili tangu Machar awekwe kifungo cha nyumbani Par sasa ametoa wito kiongozi huyo na wanachama wengine wakuu wa SPLM-IO ambao walizuiliwa kufuatia ghasia mbaya kaskazini mwa nchi waachiliwe huru.
“Kitendo hiki cha kuwekwa kizuizini kinadhoofisha kanuni za amani na mazungumzo muhimu kwa ukombozi wa taifa letu,” alisema.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukionya kuwa Sudan Kusini iko kwenye ukingo wa kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kufuatia kuongezeka kwa mzozo kati ya Machar na rais ambao umeendelea kwa wiki kadhaa.
Viongozi hao wawili walikubaliana mnamo Agosti 2018 kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoua karibu watu 400,000.
Lakini katika kipindi cha miaka saba iliyopita uhusiano wao umezidi kuwa mbaya huku kukiwa na mivutano ya kikabila na ghasia za hapa na pale.