Stevo Simple Boy adai msamaha kwa Kiengei

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki Stevo Simple Boy sasa anataka msamaha kutoka kwa Askofu wa kanisa la JCM Benson Gathungu maarufu kama Muthee Kiengei.

Tangazo la Simple Boy linajiri siku chache baada ya aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy kumsamehea Kiengei kwa maneno aliyotamka ya kumkejeli kulingana na maumbile yake.

Video ya mahojiano ya Kiengei na mmoja wa watangazaji wa runinga yake ilisambaa mitandaoni ambapo alionekana akiwa mwenye furaha akiwakejeli Simple Boy na Vishy.

Alisema Simple Boy huimba kama mbuzi suala ambalo marafiki wa mwanamuziki huyo hawakubaliani nalo kama vile mchekeshaji 2mbili.

2mbili ambaye alionekana kwenye video ya Simple Boy ya kudai msamaha alisema kwanza Kiengei anastahili kuomba Mungu msamaha kabla ya kumwomba rafiki yake.

Iwapo atakosa kuomba msamaha, 2mbili na simple Boy wametishia kuhamasisha mashabiki waandamane hadi kwenye kanisa la Kiengei ili aombe msamaha wakiwepo.

Vishy pia alikuwa ametishia kwenda kwenye kanisa hilo lakini moto huo ukazimwa haraka na Kiengei wakapatana kisha akamsaidia kupata kazi kadhaa za matangazo ya kibiashara.

Kulingana na 2mbili, Simple Boy ni mwanamuziki bora ambaye ana talanta ikitizamiwa tamasha ambazo ameandaa katika sehemu mbali mbali na wingi wa mashabiki.

Alizungumzia pia jinsi nyimbo za Simple Boy zinachezwa na kusikilizwa kote nchini na hata nje.

Share This Article