Shule ya wavulana ya St.Joseph, Kitale, imepata ushindi wa kwanza wa mabao matatu kwa nunge dhidi ya Highway kwa mashindano ya Afrika Mashariki baina ya shule za upili yanayoendelea mjini Mbale nchini Uganda.
Magoli hayo yalitingwa na J.Karia na Austine Wekesa aliyefunga mawili. Ushindi huu wa mechi ya tatu unajiri baada ya timu hiyo kutoka sare ya yai kwa yai dhidi ya Benjamin Mkapa (Tanzania) na wenyeji Bukedea.
ili timu hiyo ifuzu kwenye nusu fainali ya Jumapili, lazima ishinde mchuano wa kesho ma wa mwisho dhidi ya mabingwa watetezi St. Mary’s Kitende ( Uganda). Highway vile vile watakuwa na mulima wa kukwea dhidi ya Bukedea.
Waakilishi wengine wa Kenya – Musingu, pia walipata ushindi wa pili walipoicharaza APE Rugunga (Rwanda) magoli mawili kwa sufuri yaliyofungwa na Derrick Oketch na Harrison Amalemba.
Katika mchezo wa vikapu wa akina dada, St.Joseph iliilaza Kitende vikapu 17 Kwa 15, nayo Raila Education Centre ikalemewa vikapu 19 kwa tano na St.Noa (UG), sawia na wavulana wa Agoro Sare waliopoteza kwa alama 65 dhidi ya 66 za Hope (UG).
Kwenye mpira wa wavu, vipusa wa Moi Kamusinga waliwazaba Kiziguro (RW) alama 24 kwa 18 nao Wavulana wa Adegi ( RW) wakalipiza kisasi dhidi ya Hospital Hill alama 28 kwa 16.
Kwa upande wa raga ya wachezaji 15 kila upande, All saints Embu itachuana hapo kesho kwenye finali na St. Mary’s Kisubi (UG) baada ya kukipiku chuo cha anuai cha Maekere (UG) alama 21 kwa 17 katika nusu fainali. St.Mary’s nao walishinda Kitondo (UG) alama 39 kwa tatu.
Kwenye nusu fainali ya raga ya wachezaji saba kila upande, Vihiga watatifua kivumbi dhidi ya wakenya wenzao – St.Mary’s Yala, wakati mabingwa wa taifa – Bwake, wakimenyana na Jinja SS (UG)
Kule School of Hygiene, St.Antony(KE) watakabana na Musingu kwa nusu fainali ya magongo, Kisha St.Charles (KE) izichape na Ntare (UG). Vidosho wa St. Joseph nao watapeperusha bendera ya Kenya dhidi ya Namagunga (UG).