Spika wa bunge la taifa Moses Masika Wetang’ula, leo Jumamosi amewaongoza wabunge kumuomboleza waziri wa zamani na aliyekuwa mbunge wa Alego Usonga Peter Castro Oloo Aringo, aliyeaga dunia Ijumaa.
Katika rambirambi yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Wetang’ula alimtaja marehemu Aringo kuwa kiongozi shupavu, aliyejitolea kuhudumia taifa hili kwa bidii.
Wetang’ula, aliyehudumu na Oloo Aringo katika bunge la sita, alisifia michango yake katika maendeleo ya taifa hili.
“Huduma zake kwa raia wa Kenya zilikuwa za kujitolea mhanga hasaa katika kutatua maswala muhimu, sio tu kwa wakazi wa Alego Usonga, lakini kwa taifa nzima kwa jumla,” alisema Wetang’ula.
Spika Wetang’ula alimpongeza Aringo kwa kufanikisha kubuni tume ya kuwaajiri wafanyakazi wa bunge PSC, ambayo imetekeleza jukumu muhimu la kushughulikia maslahi ya wafanyakazi wa bunge.
“Mimi kama spika wa bunge na mwenyekiti wa tume ya PSC, ninamuenzi Oloo Aringo kwa juhudi zake za kubuni tume ya kuwaajiri wafanyakazi wa bunge, ambayo imedumisha uhuru wa kikatiba wa bunge,” alisema Wetang’ula.
Aidha, spika huyo alidokeza kuwa Aringo alitekeleza jukumu kubwa kufanikisha mfumo wa elimu wa 8-4-4, pamoja na kupiga jeki taasisi za elimu za kiufundi kote nchini.
Aringo pia alikumbukwa kwa kuwasilisha bungeni miswada iliyosababisha vyuo vikuu vya Moi, Maseno na Egerton kuwa vyuo vikuu vya umma.
“Kwa niaba yangu na bunge la taifa, natuma risala za rambi rambi kwa familia ya mheshimiwa Aringo. Mwenyezi Mungu awafariji wakati huu mgumu wa majonzi, roho yake ilazwe mahali pema,” aliomboleza Wetang’ula.