Spika Wetang’ula akutana na balozi wa EU nchini Kenya Henriette Geiger

Tom Mathinji
1 Min Read
Spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula ashauriana na balozi wa Muungano wa Ulaya hapa nchini Henriette Geiger.

Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula, leo Jumanne alishaurina na balozi wa Muungano wa Ulaya hapa nchini Henriette Geiger, aliyemtembelea afisni mwake katika majengo ya bunge.

Kupitia kwa taarifa, Wetang’ula alisema mazungumzo yao yaliangazia mkataba wa makubaliano katika ushirikiano wa kiuchumi,  kuhusu uuzaji wa bidhaa za kilimo, samaki, pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Kenya na EU.

“Makubaliano hayo yanalenga kubuni nafasi ya muda mrefu ya soko kwa bidhaa za humu nchini bila ushuru, pamoja na kupunguza ushuru kwa bidhaa zinazoingia hapa nchini kutoka Muungano wa Ulaya,” alisema Wetang’ula.

Kulingana na Wetang’ula, makubaliano hayo yatasaidia pakubwa katika ukuaji wa biashara kati ya Kenya na EU, ambao ni mshirika mkuu wa pili wa kibiashara wa taifa hili.

Kwa upande wake balozi Geiger, alisema amefurahishwa na bidii ya Kenya katika mkataba huo, ambao alisema iwapo utaptishwa utajipa jeki ukuaji wa uchumi wa taifa hili.

“Kenya itapata faida kubwa kutokana na mkataba huo ikiwa utapitishwa,” alisema Geiger.

Mwenyekiti wa kamati kuhusu biashara katika bunge la taifa James Gakuya  ambaye alihudhuria mkutano huo, alisema umma utashiriki katika kutoa maoni kuhusu mkataba huo juma lijalo, inavyohitajika kisheria.

Share This Article