Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ametoa mchango wa shilingi milioni mbili kwa timu ya soka ya Nzoia Sugar.
Wetang’ula amesema anatambua kwamba sekta ya michezo ni muhimu nchini na inahitaji kulainishwa ili vijana waweze kuchuma riziki kutokana na talanta zao.
Ameongeza kuwa mchango wake unalenga kutatua matatizo ya timu hiyo ya ligi ya NSL ili iweze kukamilisha vyema msimu huu.
Spika Wetang’ula ambaye ni shabiki wa timu ya Nzoia amemtaka mwenyekiti wake Evans Kadenge kuendeleza klabu hiyo kupitia mafunzo kwa wachezaji.
Alimhakikishia Kadenge ambaye ni mwana wa gwiji wa soka Joe Kadenge, kwamba amejitolea kusaidia timu hiyo ili kuhakikisha inaafikia malengo yake na inapandishwa ngazi hadi ligi kuu ya Kenya.
Kadenge naye alimshukuru Spika kwa usaidizi huo akiapa kuendeleza timu hiyo ipasavyo.
Mbunge wa eneo la Kanduyi John Makali alimpongeza Kadenge kwa kuelekeza vyema timu ya Nzoia, ishara kwamba vijana wana talanta zinazohitajika katika vilabu vya michezo na ambazo zinaweza kutambuliwa hasa msimu wa likizo.
Seneta Wakoli Wafula wa Bungoma aliwatia moyo vijana waweze kuangazia michezo kwani ina tija nzuri na inagharimu muda mwingi na hivyo watakuwa na cha kufanya kila wakati.