Spika Wetang’ula ahimiza uadilifu katika uteuzi wa IEBC

Spika huyo alishauri wabunge kuweka maslahi ya taifa mbele ya maslahi ya kisiasa

Marion Bosire
2 Min Read

Spika wa bunge la taifa, Moses Wetang’ula, amewataka wabunge wahakikishe uwazi na uadilifu katika uteuzi wa wanachama wapya wa tume huru ya uchaguzi na mipaka – IEBC.

Akizungumza wakati wa ibada katika Parokia ya Mokwo, eneo bunge la la Keiyo Kusini, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Spika alishauri wabunge kuweka maslahi ya taifa mbele ya maslahi ya kisiasa.

Wetang’ula alisisitiza kwamba Bunge lina jukumu muhimu katika kubuni taswira ya uchaguzi ya Kenya kwa kuidhinisha watu wenye uwezo na huru katika tume.

Alikumbusha wabunge kuwa bodi ya uteuzi tayari imetangaza orodha ndefu ya wagombea, na sasa ni jukumu lao kuhakikisha kuwa majina ya mwisho yanayochaguliwa yanawiana na maadili ya demokrasia ya nchi na kuepusha machafuko.

Spika aliongeza kusema kuwa IEBC imara na huru ni muhimu katika kudumisha uadilifu wa uchaguzi na imani ya umma katika michakato ya kidemokrasia ya Kenya.

Akiongea na waumini, Spika Wetang’ula alithibitisha msaada wake kwa uongozi wa Rais William Ruto, akitoa wito kwa viongozi kutoka pande zote za kisiasa kuzingatia umoja na maendeleo.

Aliwataka wanasiasa kukomesha mgawanyiko wa kisiasa na kufanya kazi kwa pamoja kuelekea Kenya iliyoungana, akionya kuwa kutokuwa na utulivu kisiasa kunakwamisha maendeleo.

Wetang’ula alizungumzia pia umuhimu wa kukuza viongozi vijana, akisisitiza haja ya wanasiasa wazee kuelekeza na kusaidia kizazi kijacho.

Alizungumzia alichopitia binafsi kwa kukubali mwaliko wa kiongozi kijana, Kimaiyo, badala ya kuhudhuria hafla nyingine kubwa, akisema ni muhimu kuinua vijana katika siasa.

“Hata leo, nilistahili kuwa na Rais wetu, lakini nikamwambia kuna kijana, Kimayo, amenialika kwake. Kama wazee, hatupaswi kuwadidimiza vijana hawa. Ningemwambia siji, sijui kama angekuja hapa aseme nini?” alieleza.

Spika Wetang’ula pia alizungumzia matukio ya kisiasa ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na mkutano kati ya Rais Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Alifafanua kuwa maamuzi ya kimkakati ndani ya kambi yao ya kisiasa yanachukuliwa kwa pamoja, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika uongozi.

“Katika timu yetu, kamati ya uongozi ndiyo inaamua masuala haya mazito. Hiyo kamati ni ‘Papa wa Roma,'” alieleza, akionyesha mtindo wa kufanya maamuzi kwa mpangilio.

Website |  + posts
Share This Article