Spika wa Bunge la Kaunti ya Kitui Kevin Kinengo Katisya, ametetea ushirikiano wake na viongozi wengine na serikali ya kitaifa ya Kenya Kwanza kufuatia tuhuma za usaliti.
Katisya alisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuleta maendeleo kwa wakazi wa Kitui.
Akizungumza katika mkutano wa kushirikisha umma uliofanyika katika Soko la Mukuyu, Wadi ya Tharaka, Eneo Bunge la Mwingi Kaskazini, Kinengo alipinga vikali madai ya wakosoaji.
Spika huyo alielezea kuwa wasaliti wa kweli ni wale wanaopinga maendeleo yanayoanzishwa na serikali ya Rais Dkt. William Ruto.
“Wanaopanga kuangusha viongozi wenzao kwa sababu wameamua kushirikiana na kufanya kazi na serikali ya kitaifa huenda wakajikuta upande wa walioshindwa,” alisema.
Kulingana naye, viongozi huchaguliwa na kuinuliwa na Mungu, hivyo wanastahili kuungwa mkono na kuheshimiwa.
Spika huyo alithibitisha tena kujitolea kwake pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Bunge la Kaunti kuendelea kumuunga mkono Rais Ruto ili kuleta maendeleo yanayoonekana katika Kaunti ya Kitui.
Kinengo alihimiza pia viongozi wa kisiasa kukumbatia siasa za utu uzima na kuheshimiana wanapokubaliana na wanapokosa kukubaliana.