Mwanamuziki wa Nigeria Darlington Okoye maarufu kama Speed Darlington au Akpi ameendelea kumtupia maneno mwanamuziki mwenza Burnaboy hata baada yake kukamatwa awali kwa sababu hiyo.
Video ilisambazwa mitandaoni ikimwonyesha Darlington akitumbuiza jukwaani mara anasimamisha burudani na kumtupia maneno Burna Boy.
Anasikika akimfananisha Burna Boy na mwanamuziki mkongwe wa Nigeria marehemu Fella Kuti, mwanzilishi wa Afrobeat, ambaye hakuwahi kuwaitia wenzake maafisa wa polisi hata baada ya kumkejeli.
Oktoba 4, 2024, Darlington alikamatwa na maafisa wa polisi jijini Lagos kufuatia maneno aliyoelekezea Burna Boy ambapo alijinakili video akitilia shaka tuzo za Grammy za Burna Boy.
Alimhusisha Burna Boy na mwanamuziki wa Marekani anayekabiliwa na utata P Diddy ambaye anaripotiwa kuandaa hafla za kingono na kisha kufanikisha taaluma za wasanii.
Baadaye alichapisha taarifa kuhusu mafuta ya watoto na kisha kurekodi wimbo uitwao “Baby Oil” ambao aliimba jukwaani hivi maajuzi.
Akpi alizungushwa na maafisa waliomkamata siku hiyo ambao baadaye walimzuilia jijini Abuja huku wengi mitandaoni wakilalamikia kutoweka kwake.
Ilidhibitishwa kwamba Burna Boy ndiye alimshtaki mwanamuziki huyo kwa kile ambacho kilitajwa kuwa kumchafulia jina.