Gavana wa zamani wa kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko na wenzake wawili wana kila sababu ya kutabasamu baada ya afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP kuwaondolea mashtaka ya ugaidi.
Sonko, Clifford Ouko na Benjamin Odhiambo walifika mbele ya mahakama ya Kahawa ambapo walikuwa wanakabiliwa na mashtaka hayo ambapo ilidaiwa kwamba walisajili watu wasiojulikana kwa ajili ya kutekeleza ugaidi.
Katika kesi hiyo, Sonko alikuwa analaumiwa pia kwa kuwa na vitu ambavyo vinaweza kutumika kwa ugaidi zikiwemo sare za jeshi, kinyume cha sehemu ya sita ya sheria ya mwaka 2012 ya kuzuia ugaidi.
Kosa hilo linadaiwa kutekelezwa Januari 31, 2021 katika eneo la Athi River kaunti ya Machakos.
Odhiambo na Ouko nao walidaiwa kutekeleza kosa sawia la kupatikana na mavazi yanayofanana sare za jeshi tarehe 3 mwezi februari mwaka 2021 katika eneo ambalo halikutajwa la nchi ya Kenya.
Hakimu mkuu wa mahakama ya Kahawa Daniel Kiage alisema kwamba kesi hiyo imeondolewa baada ya afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuomba mahakama kuitupilia mbali.
Upande wa utetezi pia ulikuwa umeweka ombi mbele ya mahakam hiyo kwamba Sonko na wenzake warejeshewe pesa walizotoa kama dhamana. Sonko alitoa dhamana ya laki tano huku wenzake wawili wakitoa dhamana ya shilingi laki mbili kila mmoja.