Sonko azungumzia utata kuhusu mtoto James.

Mjomba wa mtoto huyo ambaye yuko chini ya malezi ya Sonko anaripotiwa kumharibia Gavana huyo wa zamani jina.

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa zamani Mike Mbuvi Sonko amezungumzia utata unaozingira mtoto aliyeasili kwa jina James.

“Ningependa kufafanua madai yanayoendelea kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mjomba wa mtoto James anayejulikana kama Samuel Moranga Araka,” alianza Sonko katika ujumbe aliochapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Alifafanua kwamba amekuwa akimtunza mtoto huyo kama mlezi baada yake kupitia tukio la kusikitisha na lisilo la kibinadamu ambapo baba yake aliuawa mtoto akishuhudia.

“Ilikuwa katika kipindi hicho kigumu ndipo niliamua kuingilia kati kwa huruma tu. Sikuwahi kumfahamu baba yake James binafsi, lakini nilichagua kusaidia,” aliendelea kusema Gavana huyo wa zamani ambaye pia ni mhisani katika jamii.

Kulingana na Sonko, masuala mazito ya utovu wa nidhamu na ukosefu wa uaminifu yalizuka kati yake na mjomba huyo wa James ambaye alikuwa amempa ajira.

Anasema Araka alikosa kuwa mwaminifu kazini ambapo mara nyingi alikuwa akiiba pesa za matumizi ya nyumbani, jambo lililotulazimu kuchukua hatua za kinidhamu kwa kumsimamisha kazi.

Kiongozi huyo anasema inasikitisha kuona sasa madai ya uongo yakitolewa kwamba yeye amemchukua mtoto wa mtu.

“Ningependa kuweka wazi, sijawahi kumtumia vibaya au kumdhulumu mtoto yeyote. Kwa miaka mingi, nimekuwa nikisaidia na kulea watoto walio katika mazingira magumu, hasa mayatima, kama sehemu ya huduma yangu kwa jamii,” alijitetea.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao ni wafuasi wa Sonko waliotoa maoni yake kuhusiana na ujumbe huo, walimhimiza Sonko kutomwachilia mtoto James ambaye amebadilisha maisha yake pakubwa.

Sonko labda kutokana na hasira alikuwa ametishia kumwachilia mtoto huyo na kumrejesha kwa watu wa familia yake akitaja kuharibiwa jina na Araka.

Share This Article