Gavana wa zamani wa kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi almaarufu Sonko, ametoa wito kwa Rais William Ruto kurejesha mswada wa fedha wa mwaka 2024 bungeni.
Kwenye akaunti yake ya mtandao wa X Sonko aliandika, “Rafiki yangu Rais, kama hii nchi iko ndani ya roho yako na ulibeba bibilia pale Kasarani ukasema utatulinda sisi wakenya kupitia katiba, basi rejesha mswada wa fedha wa mwaka 2024 bungeni.”
Kwa upande mwingine Sonko alisifia vijana ambao walijitokeza kwa maandamano akisema wanahisi ni wakati wao na hawawezi kamwe kukwazwa katika maazimio yao.
Kulingana naye watoto wa watu tajika akiwemo wake walijitokeza jijini Nairobi kwa maandamano na hiyo ni ishara tosha kwamba wameamua huku akiongeza kusema kwamba baadhi ya wazazi wanaunga mkono wanao.
Alitaja maandamano ya jana ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024 kuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika eneo la Afrika Mashariki.
Mswada wa fedha wa mwaka 2024 ulipitisha jana alasiri katika bunge la taifa na sasa unaingia hatua ya mwisho ya kutiwa saini na Rais William Ruto ili kuwa sheria.