Somalia yapiga marufuku TikTok na Telegram

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali ya Somalia imetangaza marufuku dhidi ya mitandao ya kijamii ya TikTok na Telegram pamoja na programu moja ya kucheza kamari mtandaoni ikisema vitu hivyo vinatumika na magaidi kueneza mambo ya uongo.

Haya yanajiri wakati serikali hiyo inajiandaa kwa awamu ya pili ya mashambulizi ya wanajeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab, ambalo limekuwa likitekeleza maasi dhidi ya serikali ya nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 15 sasa.

Wizara ya habari na mawasiliano nchini humo ilitoa taarifa Jumapili ikiagiza wanaotoa huduma za mtandao kutekeleza marufuku hiyo kufikia Agosti 24 au wakabiliwe kisheria.

Taarifa hiyo ilielezea kwamba marufuku dhidi ya mitandao hiyo ya kijamii na programu ya kamari ya 1XBET inalenga kupiga jeki vita dhidi ya magaidi ambao hutumia majukwaa hayo kueneza mambo ya uongo na mengine yanayokiuka maadili.

Jeshi la Somalia limekuwa likishambulia kundi la Alshabaab tangu Agosti mwaka jana kwa ushirikiano na wapiganaji wa koo mbali mbali oparesheni inayoungwa mkono na umoja wa Afrika na Marekani.

Wanamgambo wa Al-Shabaab waliondolewa jijini Mogadishu mwaka 2011 lakini bado wanadhibiti sehemu fulani za mashinani kote nchini Somalia ambapo wanatekeleza mashambulizi dhidi ya raia, wanasiasa na hata wanajeshi.

Rais Hassan Sheikh Mohamud ameapa kuondoa kabisa wapiganaji wa makundi ya waasi nchini humo na anatarajiwa kutangaza mwanzo wa awamu ya pili ya mashambulizi wakati wowote hasa katika eneo la kusini.

Website |  + posts
Share This Article