Wizara ya Elimu imetangaza kwamba siku iliyotengwa na serikali kwa ajili ya upanzi wa miti nchini haitaathiri mtihani unaoendelea wa kidato cha nne, KCSE.
Serikali imetangaza Novemba 13, 2023 kuwa sikukuu ya upanzi wa miti.
Hata hivyo, katika taarifa, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amesema mitihani ambayo imepangiwa kufanyika siku hiyo itaendelea kama ilivyopangwa.
Waziri Machogu ameagiza maafisa wa idara mbalimbali wanaosimamia mtihani huo kufika kwenye vituo vya mtihani kama kawaida na kuendeleza shughuli.
Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki alichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali Jumatatu, Novemba 13, 2023 kuwa sikukuu ya upanzi wa miti.
Hatua hii inadhamiriwa kupiga jeki azimio la Rais William Ruto la kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.
Wizara ya Mazingira na Misitu iliandaa kikao na wanahabari leo Jumanne, ambapo Waziri Soipan Tuya aliwaomba Wakenya kujiunga na mpango wa serikali wa kutunza mazingira.
Tuya alielezea kwamba shughuli ya kitaifa siku hiyo itaandaliwa katika eneo chepechepe la Kui katika kaunti ya Makueni na kuhudhuriwa na Rais.