Wakristo kote duniani wamesherehekea sikukuu ya Krimasi Jumatano, Disemba 25 kwa ukumbusho wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwa njia tofauti.
Ilivyo ada, New Zealand ilikuwa ya kwanza kusherehekea siku hii kutokana na saa zao zilizo mbele kuliko mataifa yote ulimwenguni.
Krismasi husherehekewa na yapata watu zaidi ya bilioni mbili ambayo ni theluthi moja ya idadi ya watu ulimwenguni.
Humu nchini, sherehe za Krismasi zilianza kusherehekewa tarehe 24 na zitaendelea hadi Disemba 26 maarufu kama Boxing Dei, inayoaminika kuwa siku ambayo zawadi alizoletewa Maria, mamake Yesu, na wageni zilifunguliwa.
Krismasi ni siku ya kila Mkristo kuzaliwa upya moyoni na kukombolewa kutokana na dhambi na wengi hujumuika na ndugu, jamaa na marafiki kula, kunywa na kuburudika pamoja.
Wakenya walimiminika katika maeneo ya burudani na makanisani mapema Jumatano kwa ibada na kusherehekea siku hii maarufu.
Idadi ya wasafiri kutoka jijini Nairobi kuelekea mashinani ilikuwa ndogo zaidi ikilinganishwa na waliosafiri siku chache kabla ya Krismasi.
TWAWATAKIENI KRISMASI YA HERI NA FANAKA