Sikujiumba – Nyota Ndogo amjibu shabiki

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa eneo la Pwani Nyota Ndogo amemjibu shabiki ambaye alimtumia ujumbe wa kuumiza moyo.

Hivi maajuzi, mwimbaji huyo alitoa kibao kipya kwa jina “Kimbelembele” na inaaminika shabiki huyo alikuwa anatoa maoni kukihusu.

Nyota Ndogo alichapisha ujumbe huo ambao ni, “Sauti na sura haziambatani!! Kabisa, sauti inamtoa nyoka pangoni, lakini sura inamrudisha nyoka pangoni. Sura ni ya Ken wa Maria. Huna nguo zingine jamani.”

Shabiki huyo alisifia wimbo huo akisema hicho ndicho tu kitu kizuri kutoka kwa Nyota Ndogo.

Mwimbaji huyo alimjibu akisema hakujiumba na kwamba mume wake ambaye ni mzungu huwa halalamiki kuhusu sura yake.

Siku chache zilizopita, Nyota alitangaza kwamba yeye ni mjamzito, suala ambalo lilisababisha wengi wamtupie maneno yasiyo mazuri wengine wakihisi kwamba umri wake ulikuwa umezidi wa kupata watoto.

Mwimbaji huyo ambaye jina lake halisi ni Mwanaisha Abdalla, ana umri wa miaka 42 na hujihusisha pia na biashara ya chakula mjini Voi.

 

YouTube player
TAGGED:
Share This Article