Siku ya Moi Dei ilivyobadilika na kuwa siku ya Mazingira

Tom Mathinji
3 Min Read
Rais William Ruto aongoza zoezi la upanzi wa miti.

Siku kuu ya Moi,almaarufu Moi Dei, iliadhimishwa kwa kipindi cha takriban miongo miwili. Rais Daniel Arap Moi alichukua hatamu za uongozi wa taifa hili mnamo mwaka 1978, kufuatia kifo cha mtangulizi wake Mzee Jomo Kenyatta.

Siku kuu ya Moi ilianzishwa mwaka 1990 kama siku kuu ya kitaifa nchini Kenya, na ilisherehekewa kila mwaka tarehe 10 mwezi Oktoba, kuadhimisha siku ambayo Rais Moi alichukua hatamu za uongozi kama Rais wa pili.

Huku ikiwa sikukuu ya kitaifa, siku kuu ya Moi iliadhimishwa kwa sherehe za aina yake … Densi, umoja wa raia, michezo ya kuigiza na hatimaye hotuba ya Rais, vyote hivyo vilifanya sherehe hizo kuwa na kumbukumbu zisizo na kifani.

Walivyosema Waswahili, lililo na mwanzo lina mwisho, miaka 20 ya sherehe za Moi Dei ilifika kikomo, baada ya kupitishwa kwa katiba mpya ya mwaka 2010..Huku ikichukua muda wa takriban miaka 7 kurejesha sherehe hiyo katika kalenda ya taifa hili kupitia mahakama.

Huku ombi likiwa limewasilishwa mahakamani, Mahakama ya Upeo ilitambua siku hiyo na kuirejesha kuwa sikukuu ya kitaifa kupitia sheria ya sikukuu za taifa. Rais wa tatu wa taifa hili Uhuru Kenyatta aliidhinisha mabadiliko hayo Disemba 19,2019, na kuiita siku hiyo Huduma Dei. Siku hiyo ililenga kuimarisha utoaji huduma na kujitolea kwa hiari kutoa huduma hapa nchini.

Hata hivyo, siku hiyo haikudumu kwa muda mrefu, kwani mnamo mwaka 2020, ilibadilishwa jinana kuwa Utamaduni Dei, kupitia mswada wa bunge.

Siku hii ilikusudiwa kusherehekea tamaduni mbalimbali na turathi za taifa. NATS/ UPS …
Sherehe ya kwanza ya Sikukuu ya Utamaduni iliadhimishwa mwaka 2021, baada ya kutambuliwa rasmi na Waziri wa Usalama wa Taifa wakati huo Fred Matiang’i.

Utamaduni Dei, ilidumu muda mfupi pia kabla ya kufanyiwa mabadiliko na kuitwa MAZINGIRA DEI. Hii ilitekelezwa rasmi mwaka 2024, baada ya Rais William Ruto kutia saini kuwa sheria mswada wa marekebisho ya sheria za sikukuu za taifa, kuidhinisha siku hiyo kuadhimishwa tarehe 10 mwezi Oktoba kila mwaka.

Kutokana na hali yake ya sasa, Siku hii ya Mazingira itakuwa ni siku kwa Wakenya wote kushiriki shughuli za kutunza mazingira, kuwiana na juhudi za serikali za kulinda na kuhifadhi mazingira.

Mnamo mwezi Julai mwaka 2023, Rais William Ruto alitangaza kujitolea kwa serikali kupanda miti bilioni 15 kufika mwaka 2032. Hatua hiyo inalenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kurejesha utandu wa misitu ambao kwa sasa umedorora.

Rais aliwahimiza Wakenya kuunga mkono juhudi hizo za serikali za upanzi wa miti, akiwataka kuepuka kuendeleza shughuli zaondani ya misitu na maeneo chepechepe nchini.

Kupitia mchakato huo, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa juhudi za kuhifadhi maeneo 10,000 chepechepe zimeshika kasi.

Tunapojihusisha na upanzi wa miti, ili kuhakikisha taifa bora na lenye afya.. tusisahau safari ndefu ya Sikukuu ya Moi.

Share This Article