Kenya yachaguliwa katika Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu

Tom Mathinji
2 Min Read

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeichagua Kenya kuwa mwanachama wa Baraza la Umoja wa Mataifa la haki za kibinadamu, kuanzia Januari 1,2025.

Kenya ilichaguliwa pamoja na mataifa mengine 18 ambayo ni Benin, Bolivia, Colombia, Cyprus, Czechia, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Gambia, Iceland, Marshall Islands, Mexico, North Macedonia, Qatar, Jamuhuri Korea, Spain, Switzerland Thailand.

Katika taarifa, Umoja wa Mataifa ulisema nchi hizo zitahudumu kwa muhula wa miaka mitatu kuanzia tarehe moja mwezi Januari mwaka ujao.

Kenya ilituma ombi kuwa mwanachama wa baraza hilo Septemba 27,2024.

Nchi hizo zilizochaguliwa zinatarajiwa kudhihurusha viwango vya juu vya kutetea haki za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kutekeleza kikamilifu mifumo ya Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo Tume ya  kutetea haki za binadamu hapa nchini ilikuwa imeliandikia barua baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kupinga ombi la Kenya la kutaka kujiunga na baraza hilo.

Akizungumza katika kikao na wanahabari, naibu mkurugenzi mtendaji wa tume ya kutetea haki za binadamu nchini  Cornelius Oduor alilalamika kuwa Kenya haistahili kuwa katika baraza hilo akitoa mfano wa ukiukaji wa haki za binadamu.

Oduor alishutumu Huduma ya Kitaifa ya Polisi na taasisi nyingine za serikali kwa kuwa wahusika wakuu wa ukiukaji wa haki za binadamu na kuhusika pakubwa na dhuluma zinazofanywa kwa wakenya.

Kama sehemu ya mikataba ya kimataifa, Kenya inastahili kuheshimu, kulinda na kutimiza haki za binadamu chini ya sheria za kimataifa.

Share This Article