Siku ya Mashujaa 2024: Wingu la furaha latanda kaunti ya Kwale

Martin Mwanje
2 Min Read

Shangwe, vifijo na nderemo zimetanda katika kaunti ya Kwale, siku nne tu kabla ya kaunti hiyo kuwa mwenyeji wa Siku ya Mashujaa mwaka huu.

Hii ni mara ya kwanza kwa kaunti hiyo inayopatikana Pwani Kusini kuwa mwenyeji wa sherehe hizo za kitaifa zitakazoandaliwa Oktoba 20.

Rais William Ruto ataliongoza taifa kuadhimisha sherehe hizo zitakazohuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka kote nchini.

Kwa kaunti ya Kwale, huo utakuwa siyo tu wakati wa kuakisi mchango wa mashujaa mbalimbali katika ujenzi wa taifa, bali kwa wakazi wa kaunti hiyo, huo utakuwa ufunuo wa mambo mazuri yatakayotiririka kwenye kaunti hiyo. 

Wakati pirikapirika za kujiandaa kwa sherehe hizo za kihistoria zikishika kasi, wakazi tayari wanashuhudia kwa mboni za macho yao manufaa ya sherehe hizo kuandaliwa katika kaunti yao. Manufaa hayo ni pamoja na kuendelezwa kwa miundombinu na ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.  

“Hii ni zaidi ya sherehe; hii ni fursa ya kumulika mwanga kwenye uwezo wa kaunti hii na miradi ambayo inabadilisha eneo hili kwa kasi,” alisema Majuma Karisa Charo, mwanafunzi wa chuo katika kaunti hiyo. 

Kaunti ya Kwale iliteuliwa kuwa mwenyeji wa sherehe za Siku ya Mashujaa 2024 ambazo kaulimbiu yake ni “Nyumba za Gharama Nafuu.”  Kama nguzo muhimu ya Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi Kuanzia Chini hadi Juu (BETA), nyumba za gharama nafuu zinakusudia kuongeza umiliki wa nyumba na kupunguza uhaba wa makazi kote nchini. 

Kaunti hiyo inapiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miundombinu mikubwa ikiwa ni pamoja na ujenzi unaokaribia kumalizika wa Uwanja wa Kwale. 

Sherehe za Siku ya Mashujaa zitaandaliwa katika Uwanja wa Kwale unaokarabatiwa huku wageni 12,000 wakitarajiwa kuhudhuria sherehe hizo. 

Kulingana na katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo, ukarabati katika uwanja huo unaendelea kwa kasi huku kazi za ujenzi zikikaribia kumalizika. 

Hali ya usalama nayo inaimarishwa maradufu ikizingatiwa idadi ya wageni, wakiwemo viongozi mbalimbali, wakazi na watalii, wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe hizo.

 

Share This Article