Siasa zatawala mazishi ya mwanaharakati Phoebe Asiyo

Martin Mwanje
3 Min Read

Rais William Ruto aliwaongoza viongozi mbalimbali katika kuhudhuria mazishi ya mwanaharakati wa masuala ya kijinsia Dkt. Phoebe Asiyo.

Mazishi ya mwanaharakati huyo ambaye pia aliwahi kuhudumu kama mbunge wa Karachuonyo yaliandaliwa leo Ijumaa nyumbani kwake katika wadi ya Kibiri, kaunti ya Homa Bay.

Viongozi mbalimbali, akiwemo Gavana Gladys Wanga, Seneta Moses Kajwang, Seneta wa Siaya Oburu Oginga na Katibu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU Francis Atwoli, walikuwapo.

Oburu akitumia fursa hiyo kuelezea kuwa wataendelea kuunga mkono serikali jumuishi.

“Hatuondoki katika serikali jumuishi. Tutakuwa na Rais William Ruto hadi mwaka 2027 na nina uhakika tunaenda kujenga madaraja na nina uhakika tutafanikiwa katika malengo yetu,” alisema Oburu.

“Rais Ruto, watu wetu kwa jumla huwa waaminifu. Ikiwa wanakupenda au hawakupendi, watakwambia. Wakati fulani uliopita, ulipofanya kampeni hapa, haungeshangiliwa jinsi ilivyo kwa sasa. Hii ni kwa sababu Raila amewaambia watu wetu kuwa Rais anawapeleka Caanan.”

Atwoli akionekana kuwasuta viongozi vijana anaosema wanaonekana kuwa na pupa za kisiasa.

“Kuna viongozi wachanga vijana. Mkisema nyinyi ndio mna nywila (password) ya siasa za Kenya, mnajidanganya. Tutaikwamilia nywila ya uongozi wa Kenya 2027 na miaka mingi ijayo. Nywila iko na Raila, Mudavadi na William Ruto,” alisema Atwoli katika hatua iliyoibua cheko kubwa miongoni mwa hadhira.

Viongozi wengine, kama kiongozi wa chama cha PLP Martha Karua walimsifia marehemu Asiyo wakimtaja kuwa mwanaharakati shupavu aliyepigania haki za wanawake bila kutetetereka.

Dkt. Asiyo, ambaye aliaga dunia Julai 16, 2025  katika jimbo la North Carolina nchini Marekani akiwa na umri wa miaka 90, atakumbukwa kama mama mzalendo, aliyejitolea kuimarisha maisha ya mtoto wa kike hapa nchini.

Asiyo ambaye pia aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa chama cha maendeleo ya wanawake ametajwa na wengi sio tu kama mdhamini, bali pia nguzo muhimu kwenye masuala ya wanawake.

Alikuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kwenye baraza la wazee wa jamii ya Waluo na alitunukiwa tuzo ya Chief of the Burning Spear mnamo mwaka wa 2018, kwa juhudi zake za kutetea elimu ya mtoto msichana na usawa wa kijinsia nchini Kenya.

Alikuwa mkewe marehemu Richard Genga Asiyo.

Website |  + posts
Share This Article