Shule ya Sipili kaunti ya Laikipia yatafuta kurejeshewa pesa ilizolipia basi

Marion Bosire
2 Min Read

Bodi simamizi ya shule ya walemavu wa kusikia la Sipili iliyo katika kaunti ya Laikipia inatafuta usaidizi wa kurejesha fedha ambazo ilikuwa imelipia basi la shule lakini mpango huo wa ununuzi ukakosa kukamilika.

Mwenyekiti wa bodi hiyo Samuel Kimani Mbogo, anaelezea kwamba wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wameshirikiana na mhisani mmoja kutoka Canada kununua basi la shule lenye viti 52 miaka 15 iliyopita.

Kufikia wakati mpango huo unasambaratika, shule ilikuwa imelipa muuzaji mmoja wa magari mjini Thika jumla ya shilingi milioni 1.4 na walitarajia kuongeza milioni 4 kukamilisha malipo ya basi hilo.

Mhisani huyo anasemekana kuondoka nchini ghafla na wazazi hawakuweza kuchangisha pesa zilizosalia ndiposa wakaamua kuitisha malipo waliyokuwa wametoa ya milioni 1.4.

Muuzaji huyo wa magari anasemekana kurejesha shilingi laki nane baada ya muda wa kama miaka kumi na tangu wakati huo miaka mitano baadaye hajarejesha laki 6 zilizosalia.

Pesa hizo Mbogo anasema zilichangishwa na wanafunzi waliofanya matembezi ya kilomita yapata 20 kutoka Nanyuki hadi Sipili.

Mwenyekiti huyo wa bodi ya shule ya wasio na uwezo wa kusikia ya Sipili amezema pia kwamba ukosefu wa basi la shule ni changamoto kubwa kwani wanafunzi hawawezi kupelekwa ziara za kimasomo na hata za michezo.

Mbogo amefafanua kwamba hawajakata tamaa kuhusu kupata basi la shule litakalohudumia wanafunzi ambao ni 80 huku akiwataka wahisani kujitolea kusaidia shule hiyo.

Shule hiyo ina darasa la Junior Secondary School lakini haina mwalimu wa JSS a wanatoa wito kwa TSC kutuma mwalimu huko.

Share This Article