Taarifa ya Boniface Musotsi
Shule ya upili ya wavulana ya Kakamega ( Green Commandoes) imenyakua taji la shule nane bora almaarufu Super Eight kwa kuwanyofoa mahasimu wa jadi – St. Antony ya Kitale bao moja kwa sufuri kwenye fainali iliyosakatwa ugani Bukhungu, kaunti ya Kakamega siku ya Jumapili.
Bao hilo lilitingwa na mshambulizi matata Derrick Wanyonyi namo kipindi cha kwanza. Wakati wa ngarambe hiyo, timu hizo zilionyesha soka ya kufana yenye pasi fupi zenye ufundi halisi hivyo kusisimua umati mkubwa.
Wakati wa usubuhi, Kakamega na St. Antony zilivuna ushindi wa magoli mawili kwa sare katika nusu fainali dhidi ya Butere na Shanderema mtawalia.
Hii ni mara ya pili kwa kipute hicho kuandaliwa baada ya kile cha jijini Kisumu mwaka jana kilichovunwa na St. Antony.
Shule zingine zilizoshiriki ni Yala na shule wavulana ya kutwa ya Kisumu za eneo la Nyanza, Highway ya Nairobi na Kirangari ya eneo la kati mwa nchi.