Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani amewashauri wavuvi kusitisha shughuli zao huku kimbunga Hidaya kikitarajiwa katika Pwani ya Kenya.
Achani pia alisitisha shughuli zote katika maeneo ya bahari, ili kuzuia hatari zinazoweza sababishwa na kimbunga Hidaya.
“Huku Kimbunga Hidaya kikitarajiwa katika pwani ya Afrika Mashariki, serikali ya kaunti ya Kwale imesitisha shughuli za uvuvi baharini,” alisema Gavana Achani.
Kulingana na Achani kaunti zilizo katika pwani ya Kenya, hukumbwa na hali mbaya ya hewa, na ndio maana serikali yake imechukua tahadhari za kukabiliana na athari za kimbunga Hidaya.
Aidha alisema kamati ya kukabiliana na dharura ya kaunti hiyo, imebuniwa kushughulikia dharura zitakazotokea.
“Kamati hiyo ya dharura itakuwa makini kuhusu mfumo wa hali ya anga, huku ikishirikiana na asasu husika kukabiliana na janga lolote,” alidokeza Achani.
Zaidi ya watu 200 wamefariki kutokana na mafuriko hapa nchini, huku wengi wengi wakiachwa bila makao.