Shughuli zalemazwa katika viwanja vya ndege nchini

Tom Mathinji
2 Min Read
Wasafiri watatizika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Abiria katika viwanja vya ndege hapa nchini, wametatizika kufuatia kuanza kwa mgomo wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya safari za angani (KAWU),  kupinga  mipango ya kukodisha shughuli za viwanja vya ndege kwa kampuni ya Adani Group.    

Mgomo huo umelemaza shughuli katika viwanja vyote vya ndege hapa nchini, huku Katibu Mkuu wa chama hicho cha KAWU Moss Ndiema, akitoa wito kwa wasafiri wanaonuia kutumia viwanja vya ndege hapa nchini, kutumia mipango mbadala.

Katibu huyo Mkuu wa chama cha KAWU, kinachowakilisha wafanyakazi kutoka hlamashauri ya kusimamia viwanja vya ndege KAA, halmashauri ya kusimamia safari za ndege KCA, shirika la ndege la Kenya Airways KQ, kampuni ya Tradewinds Aviation Services na Eurocraft Agencies, kimetoa wito kwa serikali kuweka kando mipango yake ya kukodisha usimamizi wa viwanja vya ndege hapa nchini kwa kampuni ya Adani Airports Holding, yenye makao yake nchini India.

Wakati huo huo, Ndiema alisema kuwa wanachama wa chama hicho wanaitaka halmashauri ya kusimamia viwanja vya ndege nchini (KAA) na shirika la Kenya Airways(KQ), kuzingatia mkataba wa pamoja wa makubaliano ulioafikiwa na chama hicho na ambao haujatekelezwa.

Kupitia kwa barua iliyoandikwa kwa kaimu Mkurugenzi wa Mkuu wa halmshauri ya usimamizi wa viwanja vya ndege nchini Henry Ogoye na afisa mkuu mtendaji wa shirika la Kenya Airways  Allan Kilavuka, chama cha KAWU kilishinikiza kujiuzulu kwa bodi ya wakurugenzi wa halmashauri ya usimamizi wa viwanja vya ndege nchini pamoja na wafanyikazi wa shirika la Kenya Airways ambao walikuwa sehemu ya kundi lililojadili na kuafikia mkataba wa kuwepo kwa mwekezaji maalum wa kusimamia shughuli katika uwanja wa kimataifa wa ndege nchini wa JKIA.

Share This Article