Mwanamuziki wa asili ya Afrika Kusini Sho Madjozi, ambaye jina lake halisi ni Maya Wegerif ametangaza kwamba anaachana na muziki baada ya kuzindua albamu yake ijayo.
Akizungumza wakati wa mahojiano, Sho alisema kwamba uamuzi wake unatokana na changamoto ambazo amekumbana nazo katika tasnia ya muziki
Binti huyo anasema tasnia ya muziki ilivyo kwa sasa, wasanii hutumia muda mwingi kujaribu kupata uungwaji mkono na kujulikana ikilinganishwa na muda wanaotumia kwa ubunifu.
Madjozi wa umri wa miaka 32, amekiri hana uwezo wa kuendelea na mahitaji ya mitindo ya mitandaoni, vitendo vya kudumaza umma na mchezo wa kutafuta kuonekana zaidi.
Furaha ya kutengeneza muziki kulingana naye, imefunikwa na misukumo ya mauzo na vimbwanga vya tasnia.
Mwaka 2020 Madjozi alisajiliwa na kampuni ya Marekani ya Epic Records ambayo ina wasanii kama Mariah Carey na Travis Scott lakini changamoto zikawa nyingi.
Alihitajika kubadili mtindo wake wa muziki wa asili ya Xitsonga na kuingilia mtindo wa kizungu hatua ambayo hangeweza kutekeleza.
Hata ingawa ushirikiano na kampuni ya Epic ulikumbwa na changamoto, madjozi anasalia mwenye shukrani kwa kuchaguliwa kwani alikuwa msanii wa kwanza wa Afrika Kusini kusajiliwa humo.
Madjozi anasema ataangazia mambo ambayo yatatosheleza moyo wake kikweli baada ya kuondokea muziki ila hakuyataja.