Katibu katika wizara ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Edward Kisiang’ani, ameagiza wizara zote,Idara na mashirika yote ya serikali, kutoa Matangazo yao kupitia shirika la utangazaji nchini Kenya,KBC pekee.
Vile vile Katibu huyo aliagiza tume huru pamoja na vyuo vikuu vya umma kutoa matangazo yao kupitia KBC baada ya kutolewa kwa idhini kutoka shirika la serikali la kuthibiti matangazo, GAA.
Kwenye barua iliyoandikiwa tarehe saba mwezi Machi mwaka huu kwa makatibu wote wa wizara na wakurugenzi wakuu wa mashirika ya serikali, tume huru na machansela wa vyuo vikuu vya umma, katibu huyo alisema hatua hiyo ina-ambatana na azma ya serikali ya kupunguza gharama na kuhakikisha utoaji huduma bora kwa gharama nafuu.
Kisiang’ani alisema mawimbi ya shirika la KBC yanafika maeneo mengi na kwamba litawafaa vyema wale wanaotoa matangazo.
Kisiang’ani alisema serikali imejitolea kufufua shirika la KBC kwa kuweka mfumo wa kisasa utakaohakikisha linakuwa shirika bora la utangazaji barani Afrika.
Agizo hilo ilipongezwa na shirika la utangazaji nchini KBC, huku kaimu mkurugenzi wa shirika hilo akisema hatua hiyo itapiga jeki uwezo wa KBC wa kufahamisha umma maswala muhimu ya taifa.