Shindano la soka kwa waliokuwa waraibu wa mihadarati lazinduliwa

Tom Mathinji
1 Min Read

Mkewe Naibu Rais Dorcas Rigathi amezindua shindano la soka katika uwanja wa Mutuini, eneo bunge la Dagoreti Kusini jijini Nairobi linawalolenga waraibu wanaojirekebisha na waliorekebisha tabia kutokana na uraibu wa pombe na mihadarati.

Timu zinazoshiriki zimebuniwa kutoka kwa baadhi ya wanaume walionufaika na mpango wa kumnusuru mtoto wa kiume, unaodhaminiwa na Dorcas katika sehemu mbalimbali humu nchini.

Baadhi ya wanaume ambao hawakuwa wameathirika zaidi na uraibu wa dawa za kulevya, waliwekwa kwenye mpango wa mwezi mmoja wa urekebishaji tabia katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Jamhuri jijini Nairobi.

Kundi jingine lilinufaika na mpango huo uliodumu kwa miezi mitatu katika vituo mbalimbali vya urekebishaji tabia humu nchini.

Akiongea baada ya kulizindua,  Dorcas alisema shindano hilo linanuia kuimarisha vita dhidi ya uraibu wa pombe na mihadarati kote nchini.

Aidha, aliwapongeza wanaume walionufaika na mpango huo akiwahimiza wasikate tamaa maishani.

Share This Article