Miezi mitatu tu baada ya kupitishwa kwa sheria kali dhidi ya mashoga nchini Uganda, makali ya sheria hiyo yameanza kuhisiwa. Mwanaume mmoja wa umri wa miaka 20 amekuwa raia wa kwanza wa Uganda kushtakiwa mahakamani kwa kosa la ushoga uliokithiri.
Adhabu ya kosa hilo ni kifo.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni alitia saini sheria hiyo Mei, 2023 kinyume na matarajio ya mataifa mengi ya magharibi pamoja na mashirika ya kutetea haki.
Kulingana na sheria hiyo watu ambao watapatikana wakishiriki ngono ilhali ni wa jinsia moja watahukumiwa kifungo cha maisha gerezani huku watakaopatikana na makosa yanayochukuliwa kuwa ushoga uliokithiri wakihukumiwa kifo.
Makosa ya ushoga uliokithiri ni kama vile kurudia kosa la kushiriki ngono kati ya watu wa jinsia moja, kuambukiza mwingine ugonjwa usiokuwa na tiba, kushiriki ngono ya jinsia moja na mtoto mdogo, mkongwe au mtu mlemavu.
Stakabadhi za mahakama za Agosti 18, 2023, zinaonyesha kwamba mwanaume huyo wa miaka 20 alishiriki ngono na mwanaume wa umri wa miaka 41 bila kuelezea ni kwa nini kitendo hicho kinachukuliwa kuwa ushoga uliokithiri.
Wakili wa mshtakiwa kwa jina Justine Balya, anaamini sheria hiyo ni kinyume cha katiba ya Uganda akisema kesi ya kuipinga imewasilishwa mahakamani lakini majaji hawajaishughulikia.
Balya anasema watu wanne wameshtakiwa chini ya sheria hiyo tangu ilipopitishwa miezi mitatu iliyopita lakini mteja wake ndiye wa kwanza kuhukumiwa.
Hakuna mtu ameuawa na serikali ya Uganda kwa muda wa miaka 20 sasa lakini adhabu ya kifo haijafutiliwa mbali. Mwaka 2018, Rais Museveni alitishia kuanzisha tena matumizi ya adhabu hiyo ili kupunguza uhalifu.
Sheria hiyo dhidi ya ushoga imesababisha Uganda kutishiwa na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa ya misaada huku benki ya dunia ikisitisha misaada ya kifedha kwa taifa hilo la Afrika mashariki.
Marekani nayo imeweka vikwazo vya utoaji wa visa kwa viongozi fulani katika serikali ya Uganda wakati ambapo Rais Joe Biden ameagiza kutathminiwa upya kwa misaada kwa Uganda.