Kenya leo Ijumaa inajiunga na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Sherehe za kitaifa kuadhimisha siku hiyo zinafanyika katika kaunti ya Embu na zinaongozwa na Rais William Ruto.
Maudhui ya mwaka huu ni “Wekeza kwa Wanawake; Harakisha Maendeleo.”
Rais Ruto amewalimbikizia sifa wanawake humu nchini akisema wametekeleza wajibu muhimu katika kuchochea maendeleo ya nchi.
Ametoa mfano wa Gavana wa zamani wa Kitui Charity Ngilu na Magavana wa sasa Anne Waiguru wa Kirinyaga na Cecily Mbarire wa Embu.
Isitoshe, amesema utawala wake uko tayari kuhakikisha sheria ya theluthi mbili kwa wanawake inatekelezwa kikamilifu.
Sheria hiyo inalenga kuhakikisha kuna usawa wa kijinsia katika nyadhifa za uongozi nchini.
Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa katika kuwatakia wanawake duniani siku yenye furaha tele ameitaka jamii kusherehekea wajibu muhimu wanaotekeleza katika kuhakikisha ustawi wa jamii.
Viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula wamewatakia heri wanawake wanaposherehekea siku hiyo.