Sheila Gashumba atangaza ziara nchini Kenya

Itaanza Oktoba 8 hadi 11 anapotarajiwa kutumbuiza na kuzuru kumbi nne maarufu za burudani jijini Nairobi.

Marion Bosire
1 Min Read

Mtu maarufu katika vyombo vya habari na tasnia ya burudani nchini Uganda, Sheila Gashumba, anayefahamika zaidi kwa jina la Lil Stunner, ametangaza ziara ya siku nne jijini Nairobi, nchini Kenya.

Mrembo huyo ameahidi mashabiki wake burudani za usiku kwa siku kadhaa.

Ziara hiyo, aliyoipa jina la “Kenya Nairobi Tour”,  itafanyika kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 11, huku Gashumba akitarajiwa kutumbuiza na kuzuru kumbi nne maarufu jijini Nairobi.

Atazindua ziara hiyo Alhamisi, Oktoba 8, katika eneo la burudani la Ceil Lounge, Fortis Tower, kabla ya kuelekea 11:11 Night Club iliyopo Broadwalk Mall siku ya Ijumaa, Oktoba 9.

Jumamosi, Oktoba 10, Gashumba ataendeleza shamrashamra katika Black Samurai Lounge, Maralal Oasis na kumalizia ziara hiyo kwa hafla katika Monaco Lounge & Day Club siku ya Jumapili, Oktoba 11.

Tangazo hilo, lililotolewa na Wave Africa, linamtambulisha Gashumba kama “Lil Stunner” na kuwaalika mashabiki nchini Kenya kushiriki katika ziara hiyo.

Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha uhusiano wa msanii huyo wa Uganda na mashabiki wake nchini Kenya, huku ikiunganisha muziki, burudani za usiku na burudani kwa ujumla jijini Nairobi.

Share This Article