Bodi ya Hakimiliki ya Kenya, KECOBO imesitisha kwa muda leseni ya kuhudumu ya Chama cha Watayarishaji wa Muziki nchini Kenya, KAMP kwa miezi mitatu kuanzia Julai 1, 2026.
KAMP inatuhumiwa kwa kusimamia vibaya fedha za mirabaha, kushindwa kutekeleza maagizo ya mdhibiti na kukiuka matakwa ya utawala bora.
Katika taarifa iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KECOBO, Joshua Kutuny, bodi hiyo ilisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya utathmini wa kina kuhusu mfumo wa uongozi wa KAMP, usimamizi wa fedha, utoaji wa leseni na uzingatiaji wa sheria na kanuni.
Kutuny alisema KAMP imeshindwa kutekeleza wajibu uliotokana na makubaliano yaliyotiwa saini mwezi Juni mwaka jana kati ya KAMP na Chama cha Haki za Utendaji na Sanaa za Sauti na Taswira cha Kenya, PAVRISK, yaliyolenga kuoanisha shughuli za utoaji wa leseni.
“Ingawa KAMP ilipatiwa muda wa kutosha kutekeleza makubaliano hayo, haijayatekeleza wala kuonyesha hatua zozote za maana kuelekea kutimiza ahadi zilizomo kwenye makubaliano hayo,” alisema Kutuny.
Mirabaha ya thamani ya shilingi milioni 5.5 iliyopaswa kusambazwa kwa wenye haki ilitumika katika shughuli zisizo za msingi, kinyume na wajibu wa kisheria wa shirika lenye leseni ya usimamizi wa pamoja wa hakimiliki.
KAMP inadaiwa pia kushindwa kuzingatia kanuni ya lazima ya ugawaji wa mirabaha ya asilimia 70 kwa wenye haki na asilimia 30 kwa gharama za uendeshaji.
Hali hiyo ilisababisha fedha za mirabaha kubakizwa na kutumika isivyo halali, jambo lililowaathiri wamiliki wa haki ambao KAMP imepatiwa mamlaka ya kuwawakilisha.
KECOBO sasa imeiamuru KAMP kusitisha mara moja shughuli zote zinazohitaji leseni ya usimamizi wa pamoja wa hakimiliki chini ya Sheria ya Hakimiliki ya mwaka 2001.