Shambulio la gari na bunduki la New Orleans, Marekani lililofanyika kwenye barabara ambapo sherehe za mwaka mpya zilikuwa zikifanyika limewaua watu 15 huku wengine 35 wakijeruhiwa. Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI linasema inaamini mshukiwa wa shambulio hilo hakutekeleza shambulio hilo peke yake.
FBI ilitangaza kuwa tukio hilo lilikuwa la kigaidi na kwamba bendera ya ISIS ilipatikana kwenye gari lililokuwa likiendeshwa na mshambuliaji huyo mzaliwa wa Marekani.
Jina la mshambuliaji huyo lilitangazwa kuwa Shamsud Din Jabbar.
Pia ilibainika kuwa Jabbar, ni raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 42 kutoka Texas, na alikuwa mwanajeshi mstaafu.
FBI pia imebaini kuwa mshambuliaji “hakufanya kazi peke yake.”
Mshambulizi huyo alilenga watu wanaosherehekea Mwaka Mpya kwenye Mtaa wa Bourbon kwa lori nyeupe.
Walioshuhudia waliripoti kwamba lori hilo lilipitia vizuizi vilivyofunga barabara kwa trafiki na kuwaingia watu.
Lori la kubebea mizigo lililotumika katika tukio hilo ni aina ya Ford ya “150 Lightning”. Magari haya ni tulivu zaidi kuliko matoleo ya injini ya petroli.
Je Rais Biden amesemaje?
Rais wa Marekani Joe katika hotuba ameliita shambulio hilo “la kuchukiza”.
“Kwa familia zote za wale waliouawa, kwa wale wote waliojeruhiwa, kwa watu wote wa New Orleans ambao wanaomboleza, nataka mjue nina huzuni pamoja nanyi,” asema.
Rais Biden pia alisema wachunguzi wanachunguza iwapo shambulio la New Orleans linahusishwa na mlipuko wa lori uliotokea nje ya Hoteli ya Trump iliyopo Las Vegas saa chache zilizopita.
“Hadi sasa, hakuna cha kuripoti… kwa wakati huu,” alisema.
Aliongeza kuwa ameagiza “kila rasilimali” zipatikane kwa ajili ya utekelezaji wa sheria na kuwataka polisi wa kukabiliana na ugaidi “kuhakikisha kuwa hakuna tisho lililobaki kwa watu wa Amerika”.
Taarifa ya BBC