Shalkido alazwa hospitalini baada ya ajali

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Gengetone Shalkido, amelazwa hospitalini baada ya kupata ajali ya pikipiki kwenye barabara kuu ya Thika jijini Nairobi.

Shalkido anaripotiwa kuwa katika hali mbaya kufuatia ajali hiyo ya jana Jumapili asubuhi, na taarifa za tukio hilo zilitolewa na mwanamitandao maarufu Oga Obinna, mmoja wa watu wa mwisho kukutana na mwanamuziki huyo kabla ya tukio.

Ripoti za mwanzo zilionyesha kwamba ajali hiyo ilitokea saa 10 alfajiri, saa kadhaa baada yake kutumbuiza katika eneo moja la burudani mjini Thika.

Kulingana na Obinna, msanii huyo aliamua kusafiri kutoka Thika kurejea Nairobi akitumia pikipiki lakini saa kadhaa baadaye ripoti zikaibuka kwamba yuko hospitalini katika hali mbaya.

Obinna alielezea kwamba walipokuwa wakitoka walipoteleana na msanii huyo kisha wakapatana kwenye makutano ya barabara inayoingia Thika.

Anasema walipokutana alimwekea msanii huyo mafuta kwenye pikipiki yake na wakaendelea na safari kunako saa kumi alfajiri.

“Tulipopita chuo kikuu cha Kenyatta kidogo tu, alitupungia mkono kisha akachukua barabara ya kuondoka kwenye ile kuu ya Thika, sisi tukaendelea na safari” alielezea Obinna.

Saa kadhaa baadaye Obinna alipokea taarifa za ajali hiyo na akafahamishwa kwamba Shalkido alikimbizwa kwenye hospitali iliyokuwa karibu na sasa amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.

Ajali hii imetokea miezi michache tu tangu Shalkido arejelee kazi kama msanii baada ya kulalamikia hali yake mbaya ya kifedha.

Website |  + posts
Share This Article