Shakira atangaza kutatuliwa kwa kesi dhidi yake nchini Uhispania

Marion Bosire
2 Min Read

Shakira Isabel Mebarak Ripoll mwimbaji wa Columbia maarufu kwa jina lake moja “Shakira” ametangaza kwamba mzozo wa muda mrefu kuhusu ushuru kati yake na serikali ya Uhispania umetatuliwa.

Mwimbaji huyo wa umri wa miaka 46 alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la kukwepa kulipa ushuru na alifika mahakamani huko Barcelona kwenye siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa kesi dhidi yake.

Viongozi wa mashtaka walidai kwamba Shakira alikosa kulipa ushuru wa zaidi ya Yuro milioni 14.5 kati ya mwaka 2012 na 2014.

Katika mkataba ulioafikiwa, Shakira alikubali makosa dhidi yake na faini ya asilimia 50 ya pesa alizodaiwa kukosa kulipa kama ushuru ambazo ni takriban Yuro milioni 7.3.

Alikubali faini nyingine ya Yuro 438,000 ili kufuta adhabu ya kifungo cha miaka mitatu gerezani kulingana na jaji.

Viongozi wa mashtaka walikuwa wanataka mwanamuziki huyo ahukumiwe kifungo cha hadi miaka minane gerezani na alipe ushuru anaodaiwa.

Shakira alikaa kwa zaidi ya nusu mwaka nchini Uhispania kati ya mwaka 2012 na mwaka 2014 na kama mkazi wa nchi hiyo alitakiwa kulipa ushuru.

Shakira alishinda tuzo tatu chini ya tuzo za Grammy za Latin wiki jana ambapo alisema kwamba katika maisha yake amekuwa akijitahidi kufanya mambo kwa njia sawa na kuwa mfano mwema kwa wengine.

Katika kesi hiyo Shakira alisema kwamba amekuwa akipata ushauri kutoka kwa kampuni tajika za masuala ya ushuru ambazo ni Price waterhouse Coopers International na Ernst & Young Global.

Alisema kwamba maafisa wa serikali ya Uhispania walimfanyia kitu ambacho wamekuwa wakifanyia watu wengine wakiwemo wanariadha na watu wengine maarufu suala linalokera mno.

Badala ya kuendelea na kesi hiyo ambayo ana imani kwamba angeibuka mshindi Shakira anasema aliamua kusuluhisha suala hilo kwa njia nzuri akiwaza kuhusu watoto wake ambao alisema hawafai kushuhudia akiweka kando maslahi yake.

Share This Article