Shabana FC imechupa hadi nafasi ya saba ligini baada ya kusajili ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AFC Leopards, katika mojawapo wa mechi moja ya Ligi Kuu ya katikati mwa wiki iliyopigwa leo alasiri katika uwanja wa Gusii.
Kiungo Brian Michira alitikisa nyavu kwa Shabana ndani ya muda wa dakika nne ,dakika 34 na 38, huku Ingwe wakikomboa moja na Boniface Munyendo dakika ya 44.
Mchuano huo ulisitishwa kwa muda kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha .
Ushindi huo ulikuwa wa tatu mtawalia kwa Shabana ambao walianza kwa kuipiga Police FC na Murang’a Seal bao moja bila jibu kila moja.
Kwenye matokeo mengine ya Jumatano Posta Rangers iliwakung’uta Bidco United 3-1,Tusker FC ikawazaba Murang’a Seal 2-1 nao Gor Mahia wakaibwaga Kakamega Homeboyz 2-0.
Bandari FC wakiwa nyumbani wameilemea Kariobangi Sharks 2-0,Talanta FC wakaimenyana Ulinzi Stars bao moja kwa nunge, huku Nairobi City Stars wakaibuka kidedea bao mopja bila jawabu dhidi ya Mathare United.