Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kuwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) itazipiga dafrau changamoto si haba inazokumbana nazo kwa sasa na kutoa huduma bora kama ilivyotazamiwa.
Ruto amesema serikali itahakikisha lengo la upatikanaji wa afya kwa wote (UHC) linatimia, akisema lengo hilo lilikosa kuafikiwa na serikali za awali.
Hata hivyo, amewatahadharisha Wakenya kuwa baadhi ya changamoto zinazokumba SHA huenda zikachukua muda kuzitatua kwa sababu ya ukubwa wa mpango huo.
“Huo ni mpango mkubwa zaidi tulio nao nchini. Huenda ikachukua muda kwa mambo kutengemaa, lakini niamini: mpango huo utafanya kazi,” aliahidi kiongozi wa nchi.
Akizugumza katika eneo la Roysambu, kaunti ya Nairobi jana Jumapili, Rais Ruto alisema mpango huo wa bima ya afya unalenga kuhakikisha kila Mkenya anapata bima ya afya bila kujali hadhi yake katika jamii.
Hii ni kinyume cha siku zilizopita ambapo bima hiyo ilitumiwa tu na watu walioajiriwa au waliokuwa na uwezo wa kuigharimia.
Hakikisho lake linakuja wakati ambapo kumekuwa na lalama kutoka kwa Wakenya kuhusiana na utendakazi wa mpango huo kiasi kwamba wanalazimika kutumia fedha zao kugharimia matibabu yao.
Kwa upande mwingine, hospitali za kibinafsi zimesitisha matumizi ya mpango huo zikilalamikia hatua ya serikali kutolipa madeni yake ambayo kima chake ni shilingi bilioni 30.
Hali hiyo imesababisha hospitali za umma kuelemewa kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaotafuta matibabu.
Mpango wa SHA ulizinduliwa mwezi Oktoba mwaka jana ili kuchukua mahali pa iliyokuwa Hazina ya Bima ya Taifa ya Afya (NHIF).