Msemaji wa serikali Isaac Mwaura ameainisha hali ya uchumi wa Kenya na mabadiliko yatakayotekelezwa chini ya mpango wa ‘Bottom-Up’.
Alikuwa akizungumza na wanahabari leo Novemba 11, 2024 katika jumba la KICC.
Kulingana naye, mtazamo mpya wa serikali kuhusu kuunda nafasi zaidi za ajira, mgao wa mapato na ustawi wa kiuchumi unalenga kutoa mazingira bora ya ukuaji kwa wakenya wote huku nchi ikikabiliwa na deni la taifa na changamoto nyingine za kifedha.
“Tunatoa kipaumbele kwa sera faafu za kifedha ambazo zinawiana na maono yetu ya uchumi jumuishi.” alisema Mwaura huku akiangazia haja ya hatua za usawa za utozaji ushuru ambazo haziwaongezei wakenya mzigo.
Serikali imeanzisha sheria mpya za ushuru za kuhakikisha usawa wa ushuru katika sekta zote za jamii ambazo ni pamoja na namna ya kuondolea watu ushuru na utahmini wa kina wa matumizi ya ushuru yanayokuwa kikwazo katika ufadhili wa huduma za serikali.
Kulingana na serikali, mpango uliobadilishwa wa ukusanyaji ushuru unatarajiwa kuboresha ufadhili wa serikali za magatuzi, mafao mazuri kwa wafanyakazi na kuimarisha michango ya hazina ya malipo ya kustaafu na bima ya afya.
Serikali inaangazia pia kushughulikia deni la taifa ambalo sasa liko katika kiwango cha asilimia 68 ya pato jumla la taifa na limepunguka kutoka asilimia 73.
Serikali imepongeza hatua zilizopigwa na mamlaka inayosimamia bima ya afya ya jamii SHA ikisema kwamba imetoa huduma bora za afya kwa wakenya wapatao milioni 14 bila kuhitajika kuongeza pesa kutoka kwa mifuko yao.
Mipango ya kilimo pia iliangaziwa na msemaji wa serikali katika hotuba yake ambapo alisema kwamba serikali imetangaza bei ya shilingi 3500 kwa gunia la kilo 90 la mahindi kutoka kwa wakulima.
“Kenya itainuka, Kenya itasimama, Kenya itanawiri kwa Umoja na Uzalendo,” alimalizia Mwaura huku Kenya ikikumbwa na changamoto mbali mbali.