Serikali yazindua kituo cha pili cha kuongoza operesheni za Maliza Uhalifu

Tom Mathinji
2 Min Read
Serikali yazindua kituo cha pili cha kukabiliana na majangili bonde la Kerio.

Serikali imezindua kituo cha pili cha kuongoza operesheni za Maliza Uhalifu katika eneo la Kerio Valley, kwa lengo la kutokomeza ujangili na uhalifu katika eneo hilo.

Huku akisifu operesheni Maliza Uhalifu ambayo imedumu sasa kwa muda wa miaka miwili, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, alisema serikali imejitolea kuwamaliza majangili wote katika bonde la Kerio na kuhakikisha usalama unadumu ili kufanikisha ustawi.

“Ili kuimarisha ufanisi, tumefungua kituo kipya katika eneo la Kirimon kaunti ya Laikipia kuongoza operesheni za kukabiliana na ujangili katika maeneo ya Baringo, Marsabit, Meru na Isiolo,” alisema Murkomen.

Murkomen alisema kikosi cha maafisa kutoka asasi mbali mbali za kiusalama wanaotekeleza operesheni Maliza Uhalifu, watawafurusha wahalifu wote katika eneo hilo, ili kuzima mashambulizi ambayo hutekelezwa na wahalifu hao.

“Tutawafurusha wahalifu ambao wamejificha katika msitu wa Mukogodo kaunti ya Laikipia, na kufanya msitu huo kuwa kituo cha kupanga shughuli za uhalifu,” alidokeza waziri huyo.

Murkomen aliyasema  hayo leo Alhamisi, wakati wa mkutano wa usalama  katika kambi ya huduma ya vijana kwa taifa ya  Kirimon.

Walioandamana na waziri huyo ni pamoja na Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, naibu Inspekta Jenerali wa polisi Eliud Lagat, Kamishna wa Rift Valley Dkt. Abdi Hassan, makamanda wa polisi na maafisa wakuu wa usalama kutoka kaunti za Samburu, Laikipia, Marsabit, Meru na Isiolo.

Website |  + posts
Share This Article